Kiongozi wa mwisho wa Afrika Kusini ya ubaguzi wa rangi ambaye pia alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel sambamba na Nelson Mandela kwa kusaidia kuhitimisha utawala wa weupe wachache anatarajiwa kupachikiwa kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo baada ya kuugua.
Rais wa zamani Frederic William de Klerk, mwenye umri wa miaka 77 alijihisi kizunguzungu baada ya kurejea nyumbani kutoka Ulaya Jumapili iliyopita.
Alitarajiwa kupachikiwa kifaa hicho cha kurekebisha mapigo ya moyo jana kusaidia moyo wake kufanya kazi na alitarajiwa kubaki hospitalini hapo usiku huo.
Hili limekuja huku Mandela, mwenye miaka 94, akitimiza siku yake ya 25 hospitalini jana baada ya mwanzoni kuwa amelazwa kwa kujirudia maambukizi kwenye mapafu yake.
Tangu hapo, kumekuwa na hali ya sintofahamu nchini Afrika Kusini na duniani kwa ujumla kwa mtu huyo ambaye alitumikia miaka 27 kama mfungwa chini ya ubaguzi wa rangi na kisha kuibuka baadaye kujadiliana mwisho wa utawala wa wabaguzi weupe kabla ya kuwa rais.
Akiwa rais, de Klerk alimwachia huru Mandela kutoka gerezani. de Klerk na kiongozi huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi kisha wakaongoza majadiliano ambayo yalihitimisha utawala wa wabaguzi weupe.
Yeye na mkewe, Elita hapo kabla walitangaza kuahirisha ziara ya kikazi na mapumziko barani Ulaya sababu Mandela anaumwa mahututi.
Taasisi moja yenye makao makuu yake mjini Cape Town iliyopewa jina la de Klerk ilisema rais huyo wa zamani alipatwa maradhi ya kizunguzungu baada ya kurejea nyumbani Jumapili kutoka safari ya Ulaya, na kuonana na daktari wake Jumatatu.
"Alikuwa na matatizo kama hayo katika wiki za hivi karibuni na daktari wake alishauri upachikwaji haraka wa kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo.
"Atapachikiwa kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo baadaye leo (jana) na atakaa hospitalini hapo usiku mzima," taasisi hiyo ilisema katika taarifa yake.
Rais wa Afrika Kusini alitoa taarifa jana akimtakia kiongozi huyo wa zamani kupona kwa haraka.
"Tunamtakia Rais huyo wa zamani afya njema katika kipindi hiki kigumu. Wacha tumweke yeye na familia yake katika mawazo yetu na maombi," alisema Jacob Zuma.
Jumamosi iliyopita taasisi hiyo ilitoa taarifa kwa niaba ya de Klerk na mkewe, Elita, ikisema waliamua kuahirisha ziara ya kikazi na mapumziko barani Ulaya sababu Mandela anaumwa sana, na kwamba walikuwa wakimwombea kiongozi huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi aimarike afya yake.
Mandela alipelekwa hospitali moja ya Pretoria Juni 8, mwaka huu kutibiwa kile ambacho serikali ilisema wakati huo kurejea kwa maambukizi kwenye mapafu.
Tangu hapo, hali yake imeendelea kuwa tete nchini Afrika Kusini na duniani kote kwa mtu huyo aliyetumikia miaka 27 jela kabla ya kuja kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo katika uchaguzi huru mwaka 1994.
De Klerk, waziri wa zamani wa elimu ambaye alirejesha ubaguzi wa shule, alikuwa muhimu katika kipindi kigumu cha mpito ambacho kiligeuka na kuwa cha amani licha ya hofu ya kusambaa kwa mapigano ya kibaguzi.
Mwaka 1990, mwaka mmoja baada ya kuwa Rais wa Afrika Kusini, akatangaza kukitambua chama cha African National Congress, kundi lililopigwa marufuku ambalo liliongoza harakati za kupinga ubaguzi wa rangi, na kuwezesha kuachiwa huru kwa Mandela.
Alitunukiwa Tuzo ya Noble sambamba na Mandela kwa juhudi zake za kimapinduzi na kwa haraka kuamua mwenyewe kuachia madaraka.
De Klerk baadaye alishika wadhifa wa makamu wa rais wakati wa awamu moja ya miaka mitano ya Mandela akiwa rais.
Tangu kustaafu kwake kutoka maisha ya siasa, amekuwa akisafiri kila kona na kutoa mafundisho.
Taasisi yake inasema malengo yake ni kusaidia mafukara na watoto wasiojiweza, kushiriki kutatua migogoro na kulinda kikamilifu katiba ya Afrika Kusini, ambayo inasaidia kulinda haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment