Mashirika yasiyo ya kiserikali
yamefanya maandamano mengine mjini Nairobi Kenya kupinga jaribio la wabunge
kujiongeza mishahara hata baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kusema kuwa
hakuna pesa za kutosha kuwaongeza misahara wabunge hao.
Mashirika hayo yanataka wabunge
kukubali mishahara waliyowekewa na tume ya kudhibiti mishahara ya wafanyakazi
wa serikali. Kulingana na tume hiyo wabunge wanapaswa kupokea dola elfu sita
kila mwezi lakini wanataka pesa hizo kuongezwa hadi dola elfu kumi au shilingi
laki nane za Kenya.
Maandamano ya leo yanakuja siku
kadhaa baada ya baadhi ya wabunge kusema kuwa tayari wamepokea mishahara ya
shilingi lake nane na kupelekea tume hiyo kusema kuwa yeyote atakayepokea zaidi
ya laki tano atalazimishwa kulipa pesa hizo.
Pia yanakuja siku tatu baada ya
bunge kufutilia mbali sherehe zake za jubilee ambapo ilitarajiwa kuruhusu
wananchi kujionea bunge.
Mmoja wa wandaaji wa maandamano
hayo Bwana Boniface Mwangi, alisema kuwa waandamanaji walikuwa wanashinikizwa
sana kuwa wasiandamane.
Mwangi aliandaa maandamano ya
kwanza tarehe 14 mwezi Mei ambapo alileta Nguruwe nje ya majengo ya bunge na
kuwafananisha na wabunge hao kama Nguruwe ambao ni walafi.
Wakati huohuo, majaji watatu
wameteuliwa kusikiliza kesi zinapopinga hatua ya wabunge kutaka kujiongeza
mishahara
Majaji hao Isaac Lenaola, Mumbi
Ngugi na Weldon Korir, watasikiliza kesi hizo zilizowasilishwa na chama cha
mawakili nchini Kenya na mwanaharakati Okiya Omtatah.
Jaji Lenaola alisema kuwa tume
inayoshughulikia maslahi ya wabunge isidhubutu kuwalipa wabunge mishahara ya
juu kuliko iliyokubaliwa na tume ya mishahara hadi kesi hizo zitakapokamilika.
No comments:
Post a Comment