HOTUBA YA BAJETI 2013/2014.



HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA

MHESHIMIWA DKT. WILLIAM AUGUSTAO MGIMWA (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
I.                UTANGULIZI
1.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2013/14. Pamoja na hotuba hii, vimeandaliwa vitabu vinne vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato; Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali; Kitabu cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne kinaainisha makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.  Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013 ambao ni sehemu ya bajeti hii.

2.            Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki mkutano wa nane wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uongozi wake thabiti. Vilevile, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa vikao vya Bunge kwa kuongoza majadiliano vizuri bungeni.

3.            Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mapendekezo ya Bunge ya mzunguko mpya wa bajeti, Serikali imeridhia mapendekezo hayo ambayo yanatoa fursa ya kushirikisha wadau wengi zaidi na kuwezesha utekelezaji wa bajeti kuanza tarehe 1 Julai kila mwaka. Serikali imetekeleza mapendekezo hayo kwa kurekebisha muda na utaratibu wa hatua za uandaaji wa bajeti ambazo zimezingatiwa wakati wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2013/14.

4.            Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko hayo, Serikali itakuwa inatayarisha Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti mwezi Agosti hadi Oktoba kila mwaka; kuidhinisha na kusambaza Mwongozo mwezi Novemba; kuandaa rasimu za mipango na bajeti za mafungu mwezi Novemba hadi Januari; kufanya uchambuzi wa rasimu za Bajeti na kuingiza takwimu kwenye mfumo wa IFMS Mwezi Februari; kuwasilisha rasimu za Bajeti pamoja na randama kwenye Kamati za Bunge za Kisekta mwezi Machi; kuchapisha na kuwasilisha Bungeni vitabu vya bajeti mwezi Aprili; kuchambua na kuidhinisha bajeti Bungeni mwezi Aprili hadi Juni; na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zilizoidhinishwa muda wote wa utekelezaji wa bajeti.

5.            Mheshimiwa Spika, kufuatia mabadiliko hayo, Wizara zote zinatakiwa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha na kuhitimishwa na hotuba hii ya bajeti ya Serikali.

6.    Mheshimiwa Spika, Ninazishukuru Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau mbalimbali walioshiriki kufanikisha matayarisho ya bajeti hii. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi kwa kuchambua kwa kina bajeti za mafungu yote na kutoa mapendekezo. Aidha, naishukuru Kamati Maalum ya Mheshimiwa Spika kuhusu mapendekezo ya mapato ya Serikali; Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara inayoongozwa na Mhe. Mahmoud Hassan Mgimwa (Mb) na Waheshimiwa Wajumbe wengine wa Kamati hiyo pamoja na Wenyeviti wa Kamati nyingine za kisekta kwa ushauri, mapendekezo na maelekezo wakati wakichambua Bajeti hii. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo yao ambayo yamesaidia kuboresha Bajeti hii.

7.            Mheshimiwa Spika, ninampongeza kwa dhati Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), kwa hotuba yake ambayo imefanya majumuisho ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2012/13 na kutoa mwelekeo wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2013/14. Aidha, ninamshukuru Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa kuwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2012 na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14. Vilevile, ninawapongeza Mawaziri wenzangu kwa kuwasilisha hotuba za bajeti za wizara zao ambazo zimejumuishwa katika Bajeti hii.

8.            Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) na Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb), Katibu Mkuu; Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu  wa Mamlaka ya Mapato; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Viongozi wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; wakuu wa idara na vitengo pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha na taasisi zake kwa michango yao katika maandalizi ya Bajeti hii.  Ninamshukuru pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Fedha wa mwaka 2013 na nyaraka mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii. Aidha, ninamshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha nyaraka zote za Bajeti kwa wakati.

9.    Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2013/14 ni ya tatu katika utekelezaji wa Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010; na Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II). Aidha, Bajeti hii inaendelea kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015.  Madhumuni ya mipango na mikakati hii ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Vilevile, Bajeti hii inalenga kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu kupitia mfumo mpya wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ambayo italeta matokeo makubwa kwa haraka.

10.        Mheshimiwa Spika, kama ilivyoelezwa katika hotuba iliyowasilishwa na Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), kuhusu utaratibu mpya wa uibuaji wa vipaumbele vya Taifa ambavyo vitaleta matokeo makubwa na ya haraka (Big Results Now –BRN), Bajeti ya mwaka 2013/14, imedhamiria kutekeleza maeneo makuu sita yaliyobainishwa kama vipaumbele vya kitaifa. Maeneo hayo ni maji, nishati, uchukuzi, kilimo, elimu na kuongeza mapato.

11.                Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya awali, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/13, na mwelekeo wa makadirio ya mapato na matumizi kwa kipindi cha mwaka 2013/14.

  1. MAPITIO YA UTEKELEZAJI  WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2012/13
12.Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya Bajeti ya mwaka 2012/13 yalijikita katika kukuza Pato halisi la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012; kuongeza mapato ya ndani kufikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 18.0; kudhibiti mfumuko wa bei na hatimaye kuurudisha kwenye kiwango cha tarakimu moja; kuimarisha kiwango cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha pamoja na kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kwa asilimia 20 ya Pato la Taifa.

13.        Mheshimiwa Spika, maeneo mengine yaliyozingatiwa katika misingi na shabaha ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13 yalikuwa: kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia; kuimarika kwa utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti; kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo; kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma; kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za uwekezaji; kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii; kuimarisha utawala bora na uwajibikaji; na kuimarisha utaratibu wa  ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).
Sera za Mapato
14.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Sera za mapato zilizotekelezwa na Serikali zililenga kuongeza mapato ya ndani yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi ili kuimarisha uwezo wa Serikali wa kutoa huduma kwa umma na kupunguza utegemezi wa bajeti. Sera zilizotekelezwa zililenga katika kuimarisha taratibu za kukadiria na kukusanya mapato; kuboresha sheria za kodi; kuongeza matumizi ya kielektroniki katika kukusanya kodi; kupunguza misamaha ya kodi; na kuwianisha viwango vya kodi na tozo.

15.        Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba katika mwaka wa fedha 2012/13, Bunge lilipitisha sera mbalimbali za kodi ambazo zimetekelezwa na Serikali. Azma ya sera hizo ilikuwa ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kupanua wigo wa kodi, kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia kwa kiwango kikubwa matumizi ya Serikali kwa kutumia mapato ya ndani. Kwa kuzingatia azma hiyo, Serikali imechukua hatua zifuatazo katika eneo la mapato:-

i.                Kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kupitia upya mfumo wa ukadiriaji kodi, utoaji wa stakabadhi na leseni, pamoja na kuboresha viwango vya kubakiza maduhuli kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;

ii.        Kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;

iii.        Kufanya mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za Umma zinazokusanya maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;
iv.        Kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;

v.        Kupitia upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo katika majiji, manispaa, miji, wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;

vi.        Kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa ukusanyaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza mapato; na

vii.        Kujenga uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, na Wakala wa Ukaguzi wa Madini ili kuweza kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya madini, gesi na petroli.

Mwenendo wa Ukusanyaji Mapato ya Ndani
16.        Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2013, jumla ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 6,717.2, sawa na asilimia 93.2 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 7,209.2 katika kipindi hicho na asilimia 77.1 ya makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 8,714.7.  Kati ya makusanyo hayo, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 6,371.3 ambayo ni sawa na asilimia 96 ya makadirio ya kipindi hicho na asilimia 79.0 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 8,070.1 na mapato yasiyotokana na kodi yalikuwa shilingi bilioni 357.8 ikiwa ni asilimia 55.5 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 644.6.

17.        Mheshimiwa Spika, tathmini ya makusanyo ya mapato ya kodi inaonesha mwenendo wa kuridhisha ambapo hadi kufikia mwezi Aprili 2013, makusanyo ya ushuru wa forodha yalifikia shilingi bilioni 487.8, sawa na asilimia 84.6 ya kukusanya shilingi bilioni 576.7; mapato kutokana na kodi ya ongezeko la thamani yalifikia shilingi bilioni 1,965.5, sawa na asilimia 90.3 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 2,176.4. Kwa upande wa ushuru wa bidhaa, hadi kufikia mwezi Aprili 2013 jumla ya shilingi bilioni 1,050.7 zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 90.3 ya kukusanya shilingi bilioni 1,163.1. Kwa upande wa kodi ya mapato kwa makampuni, makusanyo yalifikia shilingi bilioni 2,381.9 hadi mwezi Aprili 2013, ambayo ni sawa na asilimia 105.4 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 2,260.7

18.        Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kulitokana, pamoja na sababu nyingine, na: kuongezeka kwa makusanyo ya kodi ya mapato ya makampuni; kuongezeka kwa kodi ya zuio inayotokana na malipo ya gawio katika makampuni ya madini; na ukusanyaji wa malimbikizo ya kodi. Hatua zingine za kiutawala zilizosababisha kuongezeka kwa mapato zinajumuisha: kuhakikisha mashine za kielektroniki zinatumika ipasavyo; kuendelea kuimarisha mfumo wa kusimamia vitalu vya kodi; kuboresha mfumo wa uthamanishaji bidhaa; kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipa kodi; mapato kutokana na mauzo ya hisa za kampuni ya M/S BP Tanzania; kuongezeka kwa ushuru wa bidhaa wa muda wa maongezi wa simu; na utozaji wa ushuru wa bidhaa katika bidhaa zote zisizo za petroli zinazostahili kutozwa kodi hiyo.

19.        Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio hayo, baadhi ya kodi zimeonesha mwenendo usioridhisha tofauti na ilivyotarajiwa, hasa kwenye kodi ya ongezeko la thamani, ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli na kodi ya mapato inayotokana na ajira. Aidha, uzalishaji katika baadhi ya viwanda ulipungua na hivyo kusababisha makusanyo ya ushuru wa bidhaa na kodi ya ongezeko la thamani kuwa chini ya matarajio. Vilevile, kumekuwa na ongezeko la uingizaji bidhaa kupitia njia zisizo rasmi bila kulipia ushuru na kodi.

20.        Mheshimiwa Spika, makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi yamekuwa hayaridhishi kutokana na: uwezo mdogo wa ukusanyaji na kukosa utaalam, vifaa duni na mifumo dhaifu ya ukusanyaji wa mapato ambayo inachangia katika upotevu wa mapato. Baadhi ya wakala na Mashirika bado hayachangii ipasavyo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, baadhi ya Idara ambazo zilikuwa vyanzo muhimu zimegeuzwa kuwa Wakala zilizoundwa chini ya Wizara mbalimbali hivyo kupunguza michango yake kwenye mapato ya Mfuko Mkuu wa Serikali.

21.        Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili 2013, mapato yanayokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 177.4, sawa na asilimia 49 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 362.2.

Misaada na Mikopo ya Nje yenye Masharti Nafuu
22.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Serikali ilikadiria kupata shilingi bilioni 842.5 kama misaada na mikopo ya kibajeti. Hadi kufikia Aprili, 2013 Serikali ilipata misaada na mikopo ya kibajeti ya shilingi bilioni 645.4 ambazo ni sawa na asilimia 77 ya makadirio ya mwaka. Kwa upande mwingine, shilingi bilioni 443.4 zilipokelewa kupitia mifuko ya kisekta, ikiwa ni sawa na asilimia 107 ya makadirio ya shilingi bilioni 415.1 kwa mwaka.

23.        Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi kilichoishia Aprili, 2013 ilifikia shilingi bilioni 1,235.7 ambayo ni asilimia 65 ya ahadi ya shilingi bilioni 1,899.1 kwa mwaka. Kumekuwepo na changamoto inayotokana na Washirika wa Maendeleo kuchelewa kutoa taarifa wanapotuma fedha moja kwa moja kwenye miradi husika; kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi; ucheleweshwaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi kutoka Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Serikali za mitaa; pamoja na mchakato mrefu wa ununuzi, hususan inapohusisha kupata idhini ya mfadhili (no objection).

Mikopo ya Ndani

24.        Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai hadi Aprili 2013, Serikali ilikopa shilingi bilioni 1,364.7 kutoka soko la ndani la mitaji kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva pamoja na shilingi bilioni 809.1 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mikopo ya Nje yenye Masharti ya Kibiashara
25.                Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13 Serikali ilikadiria kupata mikopo yenye masharti ya kibiashara shilingi bilioni 1,254.1, sawa na Dola za Kimarekani milioni 800 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika bajeti ya mwaka 2012/13 iliyopitishwa na Bunge lako tukufu. Hadi kufikia Mei 2013, Serikali ilipokea shilingi bilioni 947, sawa na dola milioni 600 kutoka benki ya Stanbic, na shilingi bilioni 59.2, sawa na dola milioni 37 kutoka benk ya Credit Suisse.

Sera za Matumizi
26.        Mheshimiwa Spika, Serikali ilitekeleza sera za matumizi kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13, ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini. Aidha, sera za matumizi zililenga kupunguza nakisi ya bajeti kwa kuwianisha mapato na matumizi; kuzingatia Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma; kusimamia ulipaji wa mishahara; na kuendelea kuhakiki na kulipa madai ya wakandarasi, wazabuni, watoa huduma na watumishi, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa bajeti.

27.        Mheshimiwa Spika, Serikali ilikadiria kutumia shilingi bilioni 15,191.9 katika mwaka 2012/13. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali katika kipindi hiki ulikuwa kama ifuatavyo: shilingi bilioni 10,597.1 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,594.8 zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.



Mwenendo wa Matumizi
28.        Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2013, matumizi ya kawaida bila kujumuisha malipo ya hatifungani zilizoiva (rollover) yalifikia shilingi bilioni 7,582.6, sawa na asilimia 82 ya makadirio ya mwaka. Kati ya kiasi hicho, malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali, katika wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma yalikuwa shilingi bilioni 3,209.2 sawa na asilimia 85 ya makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 3,781.1.

29.                Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Serikali iliendelea na udhibiti wa ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma. Kwa mwaka 2012/13 Serikali imekamilisha uhakiki wa watumishi na malipo ya mishahara kwenye Wizara pamoja na Sekretarieti za Mikoa. Kazi hii ilianza mwaka 2011/12 kwa kufanya uhakiki wa watumishi wa Serikali kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi zote. Matokeo ya uhakiki wa watumishi yalisambazwa kwa waajiri kwa ajili ya kuchukua hatua zinazostahili. Aidha, Serikali imechukua hatua ya kusambaza mfumo wa malipo kwa waajiri wote ili marekebisho ya mishahara, waajiriwa wapya, kuondoa watumishi wanaomaliza utumishi wao (wanaostaafu, wanaofukuzwa, wanaofariki, wanaocha kazi) yaweze kufanyika mara moja baada ya tukio hilo kutokea kwenye kituo cha kazi. Katika mwaka 2013/14 Serikali itaendelea na hatua za kudhibiti mishahara ya watumishi, ikiwa ni pamoja na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kuendelea kukagua eneo hilo.

30.                Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutoa kipaumbele katika kulipa Deni la Taifa. Katika kipindi hicho, malipo ya riba kwa mikopo ya ndani na nje yalikuwa shilingi bilioni 438.8, sawa na asilimia 79 ya makadirio ya shilingi bilioni 555.2 kwa mwaka. Malipo ya deni halisi la mikopo ya nje yalikuwa shilingi bilioni 79.0, sawa na asilimia 34 ya makadirio ya mwaka. Aidha, Serikali ilitumia shilingi bilioni 1,364 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Vilevile, matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 3,000.8 ikiwa ni asilimia 74 ya makadirio ya shilingi bilioni 4,070.9 kwa mwaka.

31.        Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2013, jumla ya shilingi bilioni 3,956.3 zilitolewa katika miradi ya maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya kutumia shilingi bilioni 4,594.8. Kati ya hizo, fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 2,277.2 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 2,280.6, sawa na asilimia 99.9. Aidha, fedha za nje zilikuwa shilingi bilioni 1,679.1 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 2,314.2 sawa na asilimia 73 ya makadirio ya mwaka.

Usimamizi wa Fedha za Umma
32.        Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13, Serikali ilianza kutekeleza mpangokazi wa miaka mitano wa kuiwezesha Serikali Kuu kuandaa hesabu kwa viwango vipya vya uhasibu vya Kimataifa (IPSAS Accrual Basis).  Kwa mara ya kwanza hesabu za Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2013 zitaandaliwa kwa kutumia viwango hivyo. Wizara imeandaa miongozo mbalimbali na kufanya mikutano elekezi ili kuwajengea uwezo wa uelewa wahasibu na wadau mbalimbali.

33.        Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti mapato na matumizi, Serikali imeandaa na kutoa miongozo ya usimamizi wa vihatarishi katika sekta ya umma pamoja na mwongozo wa uhakiki wa ubora wa ukaguzi wa ndani. Serikali pia imetayarisha mwongozo wa ukaguzi wa ndani kwa kuzingatia viwango vya kimataifa ambao unategemea kuanza kutumika rasmi Julai, 2013. Miongozo hiyo ina lengo la kuboresha utendaji kazi wa ukaguzi wa ndani.



Maslahi ya Watumishi
34.        Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Serikali iliendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kulingana na uwezo wa mapato yake kwa lengo la kuwawezesha kumudu gharama za maisha. Maeneo ambayo yalitiliwa mkazo ni pamoja na ongezeko la mshahara hasa kima cha chini, kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwenye mishahara, malipo ya mshahara kwa wakati na kuhakikisha watumishi wanalipwa mafao yao mara baada ya kustaafu.

Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
35.        Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa MKUKUTA II umeonesha mafanikio katika maeneo mengi ingawa bado kuna changamoto. Mafanikio hayo ni pamoja na kuendelea kukua kwa pato la Taifa, kuongezeka kwa mapato ya kodi, kukua kwa sekta ya fedha na mikopo kwa sekta binafsi, kuimarika kwa usimamizi wa matumizi ya Serikali na kuimarika kwa utoaji na upatikanaji wa huduma za jamii.

36.        Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kutathmini hali ya umaskini hapa nchini, Serikali imefanikiwa kukamilisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za Utafiti wa Hali ya Mapato na Matumizi katika kaya binafsi ya mwaka 2012. Uchambuzi wa takwimu hizo unaendelea na unatarajia kukamilika kabla ya Desemba 2013. Aidha, takwimu za Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika 2012, na Utafiti wa Hali ya Ajira na Kipato wa mwaka 2012 vitafanyiwa uchambuzi wa kina ili kutuwezesha kupata takwimu zitakazoonesha hali ya umaskini katika ngazi mbalimbali. Tafiti hizi zitatoa matokeo ya utekelezaji wa MKUKUTA katika nguzo ya kwanza ya Kupunguza Umaskini na Ukuaji wa Uchumi.

37.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nguzo ya pili ya MKUKUTA ya kuboresha hali ya maisha na ustawi wa jamii, viashiria vingi vilionesha mabadiliko chanya. Viwango vya uandikishaji katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari vimeimarika. Aidha, uandikishaji katika ngazi ya vyuo vya ufundi na elimu ya juu uko katika kiwango cha kuridhisha. Matokeo haya yanatokana na utekelezaji wa juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule, vyuo, waalimu, upanuzi wa miundombinu ya ufundishaji na kuongezeka kwa mikopo ya elimu ya juu. Changamoto iliyopo ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza katika ngazi zote. Katika mwaka 2012/13, Serikali iliendelea pia kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za afya, lishe, upatikanaji wa maji safi na salama na utoaji elimu kwa umma kuhusu kinga ya malaria na athari za ugonjwa wa UKIMWI.

38.        Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mali za umma, kuimarisha mfumo wa sheria na haki za binadamu, hususan katika ngazi za chini kwa kuongeza idadi ya mahakimu.  Hatua hii imeboresha kasi ya utoaji maamuzi ya mashauri katika mahakama zetu. Aidha, programu ya maboresho ya sekta ya sheria nayo iliendelea kutekelezwa, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa haki za raia zinaboreshwa na kulindwa, hususan wale walio katika mazingira hatarishi.

Sensa ya Watu na Makazi
39.                Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Serikali ilifanya Sensa ya Watu na Makazi kama ilivyopangwa ambapo jumla ya shilingi bilioni 127.3 zilitumika. Matokeo ya sensa hiyo, yalibainisha kuwa Tanzania ina jumla ya watu milioni 44.9 sawa na ongezeko la asilimia 2.6 kwa mwaka ikilinganishwa na matokeo ya Sensa ya mwaka 2002 ambapo ongezeko lilikuwa asilimia 2.9.

40.                Mheshimiwa Spika, kasi ya ongezeko la idadi ya watu ni kubwa kwa mikoa ya Dar es Salaam na Mjini Magharibi ambapo kasi ya ongezeko la idadi ya watu kwa mkoa wa Dar es Salaam ni asilimia 5.6 kwa mwaka,  wakati  Mjini Magharibi kasi hiyo ni asilimia 4.2.  Aidha, mkoa wa Dar es salaam una idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na mikoa mingine ukiwa na asilimia 10 ya idadi ya wakazi wote wa Tanzania Bara. Vilevile, wastani wa idadi ya watu kwa kaya kwa mwaka 2012 umebakia karibu sawa na ule wa mwaka 2002. Wastani ulikuwa watu 4.9 kwa kaya mwaka 2012 ikilinganishwa na watu 4.8 mwaka 2002. Napenda niwajulishe waheshimiwa wabunge kwamba Serikali inatumia takwimu za sensa hii katika kuandaa sera, mikakati, mipango na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati na mipango yake. Nashauri wadau wengine wafanye hivyo pia wakati wa kuandaa mipango ya maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa Taifa letu.
41.Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na uchambuzi wa kina wa matokeo ya Sensa ambayo yatahusisha viashiria vya kiuchumi na kijamii. Napenda nitumie nafasi hii kuwajulisha kuwa toleo linalofuata ni la mgawanyo wa watu kwa umri na jinsia katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya ambalo litatolewa mwezi Julai, 2013. Matokeo yanayofuata ambayo yanahusu viashiria vya kiuchumi na kijamii yataendelea kutolewa kama yalivyoanishwa kwenye ratiba ya usambazaji na pia katika tovuti ya Serikali.

Sekta ya Fedha
42.        Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza progamu ya maboresho ya sekta ya fedha ili kuhakikisha kwamba sekta hii inachangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Katika mwaka 2012, huduma ya sekta ya fedha ilichangia asilimia 1.8 ya pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2011. Aidha, katika kipindi hicho, sekta ya fedha ilikua kwa asilimia 13.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 10.7 mwaka 2011. Ongezeko hilo lilitokana na mafanikio ya utekelezaji wa maboresho ya sekta ya fedha ambayo yaliwezesha kuongezeka kwa idadi ya benki kutoka 49 Februari 2012 hadi 51 Februari 2013; kampuni za bima kutoka 26 mwaka 2011 hadi 28 mwaka 2012; na idadi ya SACCOS kutoka 5,424 Machi 2012 hadi 5,559 Machi 2013.

43.                Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kupunguza ukwasi nchini ambapo Benki Kuu iliongeza mauzo ya fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni pamoja na mauzo ya dhamana za Serikali. Aidha, Benki Kuu ilipandisha kiwango cha chini cha fedha zinazotakiwa kuhifadhiwa Benki Kuu kwa ajili ya akiba ya amana za serikali katika mabenki kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40, pamoja na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana na mitaji yao kwa mabenki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba, 2012. Hatua hizo zilisaidia katika kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei usiojumuisha chakula na nishati (core inflation) kutoka asilimia 8.7 Mei, 2012 hadi asilimia 7.1 Mei, 2013. Vilevile, hatua hizi zilisaidia kuimarika kwa kiwango cha ubadilishanaji wa shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani.

44.                Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya utafiti wa huduma ndogo ndogo za bima kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi walio wengi. Utafiti umebaini kwamba kiwango cha matumizi ya huduma za bima bado ni kidogo, ambapo ni asilimia 19 tu ya watu wazima wanatumia huduma hizo (hii inajumuisha huduma za bima ya afya zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya). Utafiti umebaini pia kwamba uhitaji wa huduma ndogo ndogo za bima ni mkubwa na upatikanaji wa huduma hizo utasaidia katika juhudi za Serikali za kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Serikali iliendelea kuwahamasisha wananchi ili waone umuhimu wa kujiunga na huduma za bima.

45.                Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha kampuni ya Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC) ili kuwezesha benki kutoa mikopo ya nyumba. Ili benki ziweze kupata mikopo hiyo, zinapaswa ziwe na hisa kwenye kampuni hiyo. Hadi kufikia Desemba 2012, benki 12 zimenunua hisa. Serikali kupitia Kampuni ya TMRC ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 4.2 kwa benki 12 wanachama, ambazo zilitoa mikopo 1,799 yenye thamani ya shilingi bilioni 106.2.

46.                Mheshimiwa Spika, katika kutimiza azma ya Serikali ya kuimarisha usimamizi na maendeleo ya Sekta ya Fedha, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa kuanzisha Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha ambayo ndani yake kutakuwa na kitengo cha kusimamia sekta ya huduma ndogo ndogo za fedha na kitengo cha sera za sekta ya fedha. Muundo huu mpya kwa sasa uko katika hatua ya kuridhiwa. Miongoni mwa majukumu ya idara hii ni kuandaa sera ya sekta ya huduma ndogo ndogo za fedha.

47.        Mheshimiwa Spika, katika kuhamasisha uanzishwaji wa benki za wananchi, Benki kuu imekuwa ikitoa masharti nafuu yanayohusu mtaji wakati zinapoanza. Kwa mfano, wakati benki za biashara zinatakiwa kuwa na mtaji wa shilingi bilioni 15, benki za wananchi zinatakiwa kuwa na shilingi bilioni 2. Kwa upande mwingine, Serikali imekuwa ikihimiza uanzishwaji wa SACCOS, VICOBA na benki za wananchi ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na uzalishaji.

Ununuzi wa Umma
48.        Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu limetunga Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 baada ya kubaini upungufu uliokuwepo katika Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004. Aidha, Bunge lako pia limetunga Sheria ya Ubia Na. 19 ya mwaka 2010 ambayo utekelezaji wake katika hatua ya kumpata Mbia unatumia Sheria ya Ununuzi wa Umma. Hivyo kuna haja ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 ili kuzingatia maboresho na mabadiliko yanayohitajika. Mbali na kuleta uwiano wa Sheria ya Ununuzi na Sheria ya Ubia, maboresho yanalenga kuweka misingi imara ya taratibu za kusimamia ununuzi wa umma; kufafanua majukumu ya Mamlaka za usimamizi wa ununuzi wa umma; na kuongezea madaraka ya kiutendaji Taasisi za ununuzi na zile zinazosimamia ununuzi wa umma. Aidha, maboresho yanalenga kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko ya wazabuni, na kupunguza muda wa mchakato wa ununuzi. Serikali inakusudia kufuta Sheria ya Ununuzi wa Umma na. 21 ya 2004 mara baada ya mabadiliko ya Sheria Na. 7 kukamilika na Kanuni mpya kutangazwa katika gazeti la Serikali.



Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
49.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamamia sera yake ya kushirikisha sekta binafsi ili iweze kuongeza Pato la Taifa. Katika mwaka 2012/13, Serikali ilifanya uchambuzi wa awali wa baadhi ya miradi ya PPP katika sekta za ujenzi wa barabara na bandari. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze, bandari ya Katanga, bandari ya Mwambani, na bandari ya Mtwara.

50.                Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sheria ya Ubia ya mwaka 2010, changamoto iliyojitokeza ni kuwepo kwa vitengo na ofisi nyingi zinazoshughulikia masuala ya PPP. Kwa kutambua hili, Serikali katika mwaka 2013/14 itaunganisha vitengo vya PPP na kufanya mapitio ya sheria na kanuni za ubia kwa nia ya kufanya maboresho. Aidha, katika mwaka 2013/14, Serikali imepanga kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kugharamia upembuzi yakinifu ili kuendeleza miradi ya ubia hapa nchini.

Deni la Taifa
51.                Mheshimiwa Spika, hadi mwishoni mwa Machi 2013, Deni la Taifa (likijumuisha deni la umma na sekta binafsi) lilikuwa shilingi bilioni 23,673.53 ikilinganishwa na deni la shilingi bilioni 20,276.6 Machi 2012 likiwa ni ongezeko la asilimia 17. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 18,282.02 ni deni la nje na shilingi bilioni 5,397.50 ni deni la ndani. Deni la nje, linajumuisha deni la umma la shilingi bilioni 15,203.34 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 3,078.69. Kiasi hicho cha deni la nje kinajumuisha deni halisi shilingi bilioni 16,087.43 na malimbikizo ya riba ya shilingi bilioni 2,194.59. Deni la ndani linajumuisha hati fungani za muda mrefu kiasi cha shilingi bilioni 4,261.03 na dhamana za Serikali za muda mfupi kiasi cha shilingi bilioni 1,136.48. Mikopo hiyo iligharamia miradi ya maendeleo hususan miundombinu kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopitishwa na Bunge lako tukufu.



Uhimilivu wa Deni la Taifa
52.        Mheshimiwa Spika, Serikali inasimamia deni la taifa kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Deni la Taifa pamoja na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004. Kwa kuzingatia Sheria hiyo, mwaka 2012 Serikali ilifanya tathmini ya kuangalia uhimilivu wa deni la Taifa. Napenda kulijulisha bunge lako tukufu kwamba, viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa vinaonesha kuwa, deni la Taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati. Mathalani, uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Taifa kwa Pato la Taifa ni asilimia 18.9, ikilinganishwa na ukomo wake wa asilimia 50 na kiashiria cha uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Taifa kwa mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ilikuwa asilimia 53.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 200.

Tathmini ya Uwezo wa Kukopa na Kulipa Madeni
53.        Mheshimiwa Spika, Serikali imepiga hatua kubwa katika kufanikisha zoezi la nchi kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni na ipo kwenye hatua ya kupata kampuni za kufanya tathmini. Kazi hii imepangwa kukamilika mwaka 2013/14 ambapo itawezesha nchi kukopa kwa gharama nafuu katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu. Aidha, kampuni za Tanzania nazo zitaweza kupata mitaji kwa urahisi zaidi kutoka kwenye masoko ya mitaji ya kimataifa.

Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda
54.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushiriki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC). Ushiriki wetu katika jumuiya hizi ni mojawapo ya mkakati wa kuhakikisha tunaitumia jiografia ya nchi yetu kwa kukuza uchumi.

55.        Mheshimiwa Spika, mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefikia hatua ya kuanzisha Umoja wa Fedha na majadiliano ya Itifaki hiyo yanaendelea na yanatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2013. Aidha, hatua zinachukuliwa za kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja ambapo yameainishwa maeneo katika sheria zetu yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuwezesha ushiriki wa nchi katika soko hili. Baadhi ya sheria zitakazo rekebishwa ni zile zinazohusika na taratibu za kuwezesha watanzania kuwekeza mitaji yao katika nchi za Jumuiya; lengo likiwa kurahisisha biashara ya mitaji na huduma ili kuchochea uwekezaji.

56.                Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13, Serikali iliendelea na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC, ambapo taratibu za kuridhia Itifaki ya Fedha na Uwekezaji ya SADC zimekamilika. Itifaki hii itarahisisha taratibu za uwekezaji katika nchi za SADC, kuwezesha nchi za SADC kuwianisha sera za kodi hasa eneo la vivutio vya uwekezaji. Kupitia Itifaki hii, nchi za SADC zitaweza kubuni na kutekeleza sera za kuimarisha uchumi na fedha kwa pamoja kwa lengo la kuwa na utulivu wa uchumi katika ukanda huu na hivyo kuvutia uwekezaji.  Ili kuhakikisha azma hii inatekelezwa kwa vitendo, nchi za SADC zinakamilisha utaratibu wa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo.


  1. MAFANIKIO NA CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/13
57.Mheshimiwa Spika, mafanikio na changamoto za utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2012/13 kwa kila sekta yameelezwa kwa kina katika hotuba za bajeti za wizara husika ambazo bunge lako tukufu limepata fursa ya kuzijadili na kuzipitisha. Kwa kuzingatia hilo, nitaeleza kwa kifupi baadhi ya mafaniko na changamoto hizo.

Ukusanyaji wa Mapato
58.        Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2012/13 ilitekelezwa kwa mafanikio, hususan katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi; utoaji wa huduma za jamii; kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na utengamano wa kikanda na kimataifa. Aidha, Serikali imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, hususan mapato ya kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 540 kwa mwezi kwa mwaka 2011/12 hadi shilingi bilioni 640 kwa mwezi kwa mwaka 2012/13. Pamoja na wastani huo wa mwezi, kiwango cha juu cha makusanyo kilifikiwa mwezi Desemba 2012, ambapo makusanyo ya kodi na yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 890.

Ukuaji wa Uchumi
59.                Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa limeendelea kuimarika mwaka 2012 ambapo ukuaji halisi ulikuwa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2011. Ongezeko hili la ukuaji lilitokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano, pamoja na kuimarika kwa uzalishaji viwandani kutokana na jitihada za serikali za kuhakisha upatikanaji wa umeme wa uhakika sambamba na matumizi ya nishati mbadala katika uzalishaji viwandani.

60.                Mheshimiwa Spika, sekta ya mawasiliano ndiyo ilikuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa asilimia 20.6 mwaka 2012. Pamoja na kuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji, sekta ya mawasiliano ilichangia asilimia 2.3 tu katika Pato la Taifa ikilinganishwa na sekta ya kilimo ambayo pamoja na kukua kwa kiwango kidogo ilichangia asilimia 24.7 katika Pato la Taifa mwaka 2012. Zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wamejikita katika shughuli za kilimo, hivyo hii ni sekta ambayo serikali inaitilia mkazo ili kuhakikisha kuwa inaleta mafanikio yanayotarajiwa na wengi, ikiwemo kupunguza umaskini. Serikali imefanya jitihada kubwa za kuboresha sekta hii lakini bado imeendelea kukua kwa kiwango kisichozidi asilimia 5 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

61.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo ili ikue kwa kasi zaidi na kuongeza kipato na hivyo kupunguza umaskini kwa wananchi walio wengi. Juhudi hizo zinahusisha kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua; kutoa ruzuku za pembejeo za kilimo kwa wakati zikiwemo mbolea, madawa na mbegu bora; kuondoa kodi katika zana mbalimbali za sekta ya kilimo ili kuongeza tija; kuimarisha masoko ya mazao, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na uhifadhi; na kuimarisha barabara vijijini. Aidha, Serikali itaendeleza juhudi za upatikanaji wa umeme na maji vijijini. Vilevile, Serikali itaimarisha sekta nyingine za kiuchumi zenye kutoa ajira kama vile sekta za ujenzi na uzalishaji viwandani, pamoja na kupanua wigo wa kinga ya jamii ili kuongeza ushiriki wao kwenye shughuli za uchumi na hivyo  kuinua Pato la wananchi na kuongeza kasi ya  kupunguza umaskini wa kipato.

Mwenendo wa Bei
62.        Mheshimiwa Spika, wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2012 uliongezeka kwa asilimia 16.0 ikilinganishwa na asilimia 12.7 mwaka 2011. Upandaji huu wa bei ulitokana hasa na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli katika soko la dunia na kupanda kwa bei za chakula kulikotokana na mahitaji makubwa ya chakula katika baadhi ya nchi jirani.  Ikumbukwe kwamba chakula peke yake huchangia asilimia 47.8 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika ukokotoaji wa fahirisi ya bei kwenye kapu la bidhaa za walaji, ikifuatiwa na usafiri (asilimia 9.5) na nishati (asilimia 9.2). Makundi haya ni muhimu sana katika kuchochea mwelekeo wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali. Katika kukabiliana na kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, Serikali ilichukua hatua kadhaa zikiwemo:
             i.        Kuhakikisha kuwa kunakuwa na ugavi mzuri wa chakula unaoendana na mahitaji nchini;

ii.        Kupanua kilimo cha mazao ya chakula na kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea, madawa na mbegu bora;

iii.        Kuimarisha miundombinu ya usafirishaji;

iv.        Kuimarisha upatikanaji wa umeme;  na

v.        Kupandisha kiwango cha riba ya Benki Kuu inayotozwa kwa mikopo iendayo kwa taasisi za fedha nchini kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58.

63.        Mheshimiwa Spika, hatua hizi ziliwezesha kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia 18.2  mwezi Mei 2012 hadi asilimia 8.3 mwezi Mei 2013.

Mafanikio Katika Sekta Mbalimbali
64.                Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 826.1 kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa umeme na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa ni pamoja na: kuanza ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ikijumuisha ujenzi wa kituo cha kupokelea gesi Kinyerezi; kukamilisha ujenzi na kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito katika vituo vya Ubungo - Dar es Salaam (MW 105) na Nyakato - Mwanza (MW 60); kuendeleza miradi ya umeme vijijini katika mikoa 16; na kuendeleza upembuzi yakinifu katika miradi ya Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Liganga. Aidha, hadi kufikia mwezi Desemba 2012, kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Grid ya Taifa kilikuwa MWh 5,759,756 ikilinganishwa na MWh 5,153,400 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 11.8.

65.        Mheshimiwa Spika, sekta ya maji iliendelea kupewa kipaumbele katika mwaka 2012/13 kwa kuendeleza ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 682 kupitia mpango wa vijiji kumi kwa kila Halmashauri; uboreshaji wa mamlaka za maji mijini; na ujenzi wa miundombinu ya maji, ikiwemo bomba la maji la Ruvu Chini hadi Dar es Salaam. Ili kutekeleza miradi ya maji, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 106.6 katika ngazi ya Wizara na shilingi bilioni 98.4 katika ngazi ya Halmashauri.

66.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 537.40 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya tiba, kinga na ustawi wa jamii. Fedha hizo pia zilitumika katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya; kuimarisha stadi na kujenga uwezo wa rasilimali watu; na kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya, Mlonganzila - Dar es Salaam.

67.        Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 2,421.5 katika sekta ya elimu kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali katika shule za msingi, sekondari, elimu ya watu wazima, vyuo vya ufundi stadi, na vyuo vya elimu ya juu. Baadhi ya shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na: ulipaji wa mishahara kwa wakati; kuajiri walimu wapya 27,773 (walimu 13,633 wa shule ya msingi, 14,060 wa sekondari na 80 wa vyuo vya ualimu) na kuwalipa stahili zao; kugharamia uendeshaji mashuleni (Capitation); kutoa mikopo kiasi cha shilingi bilioni 326.1 kwa wanafunzi 96,350 wa elimu ya juu; kuanza ujenzi wa maabara katika shule mbili kwa kila Halmashauri 132 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 102.3 kimetolewa; ununuzi wa vitabu vya kiada na ziada 27,159,106  kwa ajili ya shule za msingi; na kuendelea kuboresha miundombinu ya kutolea elimu katika ngazi zote nchini.

68.        Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 1,044.2 kwa ajili ya kujenga na kukarabati barabara za lami; kufanya matengenezo maalumu na ya kawaida kwenye barabara za changarawe; kuboresha barabara za wilaya pamoja na kujenga na kukarabati madaraja. Aidha, fedha hizo zilitumika kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vivuko vitatu na maegesho; kukarabati vivuko vitano; na kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga barabara na vivuko katika maeneo mengine nchini. Vilevile, Serikali iliendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara za Dar es Salaam na miji mingine mikuu ili kupunguza msongamano wa magari.

69.                Mheshimiwa Spika, sekta ya uchukuzi ilipewa jumla ya  shilingi bilioni 181.8  kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo: kuanzisha usafiri wa treni ya abiria jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari na adha ya usafiri jijini Dar es Salaam; kuboresha na kurejesha huduma za treni za abiria na mizigo katika reli ya kati na TAZARA; na kuendeleza miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege vya Songwe, Katavi, Mwanza, Kigoma na Tabora.

70.        Mheshimiwa Spika, kuhusu kuimarisha utawala bora, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 27.0 kwa ajili ya mchakato wa marekebisho ya Katiba ikiwa ni pamoja na kukusanya kura za maoni katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar na shilingi bilioni 40 kutekeleza mradi wa vitambulisho vya Taifa. Aidha, shughuli zingine muhimu zilizotekelezwa ni kukamilisha rasimu ya awali ya katiba mpya, kuchapisha nakala za rasimu ya katiba mpya na kuzisambaza kwa wadau mbalimbali nchini pamoja na kuendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba.

71.        Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na upungufu wa chakula kwenye baadhi ya maeneo nchini, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 42.87 mwaka 2012/13 zilizotumika kununua tani 53,269.70 za nafaka kwa ajili ya kuongeza chakula cha hifadhi ya Taifa. Aidha, Serikali ilisambaza chakula cha msaada kwa wananchi wenye mahitaji katika Halmashauri 47 na kuuza jumla ya tani 16,653 kwa wasagishaji wa nafaka ili kurahisisha usambazaji wa unga wa sembe  na hatimaye kupunguza mfumuko wa bei nchini. Vilevile, uzalishaji wa chakula katika msimu wa mwaka 2012/13 ulifikia tani milioni 13.34 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya tani milioni 11.97.

72.        Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, changamoto bado ni nyingi, ambazo ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vya ndani na upatikanaji wa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara kwa wakati na hivyo kuchelewa kupeleka fedha kwenye sekta husika. Changamoto nyingine ni: madai ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma wa ndani na nje; kuimarisha miundombinu; kupata thamani ya fedha katika ununuzi wa umma; kuongeza ubora na tija katika uzalishaji; kutumia fursa za kijiografia katika ukuzaji wa uchumi; upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika; riba za mikopo; kusimamia deni la Taifa; kudhibiti mfumuko wa bei na mabadiliko ya tabianchi.

73.        Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni: huduma za jamii hususan elimu, afya, na maji bado hazijafikia viwango vinavyotarajiwa; kuongeza fursa za ajira; kukuza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP); na upatikanaji wa huduma za mikopo ya kilimo. Changamoto hizo zitaendelea kutafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua katika kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Aidha, Serikali imejipanga kukabiliana na baadhi ya changamoto hizi katika mwaka 2013/14.

            IV.        BAJETI YA MWAKA 2013/14
74.Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2013/14 itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye: Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14 na mfumo mpya wa utekelezaji wa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka (Big Results Now – BRN); Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; na programu za maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Shabaha na Malengo ya Bajeti kwa Mwaka 2013/14
75.                Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2013/14, imejielekeza katika kufikia shabaha na malengo ya uchumi jumla yafuatayo:
i.        Pato halisi la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 mwaka 2013, na asilimia 7.2 mwaka 2014;

ii.        Kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja, ambapo mfumuko wa bei unatarajiwa kushuka zaidi kufikia asilimia 6.0 Juni 2014;

iii.        Kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia  20.2 mwaka 2013/14 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 17.7 kwa mwaka 2012/13;

iv.        Kuwa na nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) isiyozidi asilimia 5.0 ya Pato la Taifa mwaka 2013/14;

v.        Kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) katika wigo wa asilimia 15.0 Juni 2014  utakaowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kasi ya upandaji bei;

vi.        Kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne mwaka 2013/14;


vii.        Kupunguza tofauti ya viwango vya riba vya kuweka na kukopa; na

viii.        Kuimarisha thamani ya Shilingi na kuwa na kiwango imara cha ubadilishanaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.

Misingi ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2013/14
76.                Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo yaliyoainishwa hapo juu, misingi ya bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2013/14 ni hii ifuatayo:-

     i.        Kuendelea kuimarisha na kudumisha amani, usalama, utulivu na utengamano;

ii.        Kuendelea kuboresha viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii vikiwemo Pato la Taifa, biashara ya nje, fedha, mapato na matumizi na viashiria vya huduma za jamii;
iii.        Kuongeza mapato ya ndani kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kubuni vyanzo vipya vya mapato;

iv.        Kuboresha usimamizi wa fedha za umma;

v.        Kuimarisha mfumo wa IFMS na kuhakikisha unatumika kuweka mihadi ya huduma na bidhaa kabla ya malipo;

vi.        Kuzingatia vipaumbele vilivyopo katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano hasa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka pamoja na MKUKUTA II;

vii.        Kuboresha mfumo wa utekelezaji wa vipaumbele na uwajibikaji;

viii.        Kuendelea kuimarisha sera za fedha ili ziendane na sera za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti ya riba za amana na za mikopo; na

ix.        Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi.


Sera za Mapato

77.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali inakusudia kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mapato ya ndani yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi. Sera za mapato zinajumuisha kupanua wigo wa kodi kwa kubainisha vyanzo vipya na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vilivyopo. Aidha, hatua zaidi zitachukuliwa kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi. Kwa ujumla, sera na hatua zitakazotekelezwa katika mwaka wa fedha 2013/14 zinalenga kuimarisha uwezo wa Serikali kukusanya mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka nje, na kupunguza kutegemea kodi zinazotokana na biashara za kimataifa ambazo zimeanza kushuka kutokana na kuongezeka kwa biashara za ushirikiano wa kikanda katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.

78.                Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mikakati ya pamoja ya kuongeza mapato ya Serikali, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa hatua uliyochukua ya kuunda Kamati ya Spika ili kuishauri Serikali kuhusu vyanzo vya mapato ambapo baadhi ya mapendekezo yake yamezingatiwa katika Sera za Mapato kwenye Bajeti ya mwaka 2013/14.

79.                Mheshimiwa Spika, Serikali itatekeleza baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Labs ya kubuni vyanzo vya mapato. Baadhi ya mapendekezo hayo ni kuanza kuuza vitalu vya misitu na uwindaji kwa njia ya mnada na kufanya tathmini ya mali na ardhi ili kuimarisha makusanyo ya tozo ya mali na kodi ya ardhi. Hatua nyingine za kumairisha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi tayari zimeshatangazwa kupitia bajeti za Wizara husika.

80.                Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha wa 2013/14 itatekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ili kupunguza utegemezi. Moja ya hatua muhimu itakayotekelezwa katika mwaka 2013/14 ni kuangalia upya misamaha ya kodi kwa lengo la kuipunguza. Hatua nyingine zitakazochukuliwa ni pamoja na:

i.                Kupunguza misamaha ya kodi kwa kufuta msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye huduma za utalii. Aidha, Sheria ya Uwekezaji itafanyiwa marekebisho ili kupunguza misamaha ya kodi na kubakiza misamaha yenye tija na yenye kuchochea uwekezaji mkubwa katika sekta za uchumi za kimkakati;

  1. Kuendelea kuunga mkono jitihada za kuanzisha kituo kimoja cha kutoa huduma bandarini (one stop centre) katika bandari. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza mpango wa kuanzisha One Stop Border Posts katika mipaka kwenye vituo vya Holili, Mutukula, Sirari, Horohoro, Kabanga, Tunduma, Rusumo na Namanga;

  1. Kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali wakiwemo wa Mamlaka ya Mapato ili kupata ujuzi wa kuthibiti mbinu za kukwepa kodi zinazotumiwa na makampuni makubwa hasa katika sekta za mawasiliano, madini na gesi ukiwemo ujuzi wa kukagua uhamishaji wa gharama yaani  “transfer pricing” hivyo kudhibiti mianya ya kupotea kwa mapato;

  1. Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendela kuimarisha matumizi ya mashine za kieletroniki za kutoa risiti (Electronic Fiscal Devices-EFDs) ambazo zimeunganishwa moja kwa moja na Mamlaka kwa mtandao wa kompyuta ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata mapato yake stahiki.  Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia mtandao wa kielektroniki ambapo hupeleka moja kwa moja taarifa kwenye hifadhi kuu ya Mamlaka kila siku.

  1. Kuwajengea uwezo watumishi kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi, hususan katika sekta ya gesi, mafuta na madini ili kusimamia ipasavyo mapato yatokanayo na rasimali hizo; na

  1. Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanzisha mfumo mpya ujulikanao kama Revenue Gateway ambao utaanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 1 Julai 2013. Mfumo huo unalenga kuboresha mifumo iliyopo ya ulipaji kodi na upatikanaji wa taarifa za malipo ya kodi kwa njia ya mtandao. Aidha, mfumo huo utarahisisha uhamishaji wa fedha kutoka kwenye benki za biashara hadi Mfuko Mkuu wa Serikali.  Vilevile, mlipakodi atalazimika kujisajili kwa ajili ya kufanya malipo kupitia tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kabla ya kulipa kupitia mfumo wa Tanzania Interbank Settlement System (TISS). Mtumiaji wa mfumo huu atanufaika kwa kupata taarifa kwa njia ya barua pepe kuhusu malipo yake ya kodi aliyofanya.

81.                Mheshimiwa Spika, Sera za mapato katika mwaka 2013/14, zinalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 11,154.1 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi ni shilingi bilioni 10,412.9, na mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 741.1. Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri ni shilingi bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.

Mikopo ya Ndani
82.                Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina changamoto ya kugharamia miradi ya maendeleo kwa kutegemea mapato ya ndani. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali itakopa kutoka soko la ndani shilingi bilioni 552.3, sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, katika mwaka 2013/14, Serikali itakopa shilingi bilioni 1,147.6 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva.

Misaada na Mikopo ya Masharti Nafuu
83.        Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wamekuwa wakichangia katika bajeti ya matumizi ya maendeleo. Katika mwaka 2013/14, Serikali inatarajia kupata misaada na mikopo yenye masharti nafuu kiasi cha shilingi bilioni 3,855.2 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kati ya fedha hizo, misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 1,163.1; misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 2,191.6; na mifuko ya kisekta ni shilingi bilioni 500.  Aidha, Serikali itaendelea kusimamia matumizi ya fedha za Washirika wa Maendeleo na kuhakikisha zinaleta ufanisi na tija.

84.                Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi zao za kuchangia maendeleo yetu, naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika wa Maendeleo yetu kama ifuatavyo: Nchi za Canada, China, Denmark, Finland, Hispania, India, Ireland, Italia, Japani, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, na Uswisi, pia taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, BADEA, Global Funds, OPEC Fund, Saudi Fund, Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Tunawashukuru sana na tunathamini michango yao.


Mikopo ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
85.                Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka 2013/14 na changamoto za upatikanaji wa mapato ya ndani, Serikali itakopa kutoka nje mikopo yenye masharti nafuu ya kibiashara shilingi bilioni 1,156.4, sawa na Dola za Marekani milioni 700. Mikopo hiyo itatumika kugharamia miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14. Uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la Taifa uliopo.

Sera za Matumizi
86.                Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itatekeleza sera za matumizi zifuatazo:-
  1. Kuwianisha matumizi na mapato yanayotarajiwa;
ii.        Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haitazidi asilimia 5.0 ya Pato la Taifa;

iii.        Mafungu yatazingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;

iv.        Kutenga fedha za kutosha katika kutekeleza miradi ya vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo; na

v.        Kuzingatia Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma.

87.        Mheshimiwa Spika, matumizi ya kawaida kwa mwaka  2013/14 yanalenga katika kufanikisha maeneo yafuatayo: kugharamia nyongeza ya mishahara pamoja na kulipa mishahara kwa wakati; kuboresha huduma za kiuchumi na maendeleo ya jamii; kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuendelea na utoaji wa vitambulisho vya Taifa; kukamilisha uchambuzi wa takwimu za sensa ya watu na makazi; maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015; na kuendelea kulipa madeni ya ndani na nje yaliyoiva pamoja na madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni yaliyohakikiwa.

88.        Mheshimiwa spika, katika bajeti ya mwaka 2012/13, Serikali ililenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika maeneo mbalimbali kama vile semina, usafiri wa ndani na nje, ununuzi wa samani, maonesho mbalimbali na katika magari. Matokeo ya hatua hizi yameleta mafanikio kadhaa ikiwemo yafuatayo: semina na warsha zimepunguzwa; manunuzi ya magari mapya yamepunguzwa na yananunuliwa kwa kibali cha Waziri Mkuu tu na ukubwa wa injini umepunguzwa na kubaki zenye ukubwa uliokubalika (cc 3,000 au chini ya hapo); maonyesho pia yamepunguzwa mfano maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma hayakufanyika mwaka 2012/13; ununuzi wa samani kutoka nje umepungua.

89.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itaendelea kudhibiti matumizi yake katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutumia malipo ya simu kabla ya huduma; kutumia utaratibu wa ununuzi wa magari wa pamoja ambao utapunguza gharama za ununuzi; kupunguza matumizi ya magari ya Serikali kwa kuanzisha utaratibu wa kuwakopesha magari watumishi wa Serikali wanaostahili; kuoanisha kanuni za ununuzi wa umma za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa lengo la kuimarisha ununuzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; na kuhimiza matumizi ya samani zinazotengenezwa nchini.

90.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi ya maendeleo, bajeti itazingatia kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao mwaka 2013/14 unaingia mwaka wa tatu wa utekelezaji kama ifuatavyo:
             i.        Miundombinu: - miundombinu ya nishati; usafirishaji (barabara, reli, viwanja vya ndege, usafiri wa majini ); TEHAMA; maji safi na maji taka na umwagiliaji;
ii.        Kilimo: – ikijumuisha mazao ya chakula na biashara, malighafi ya viwandani, ufugaji, uvuvi na misitu;

iii.        Viwanda: – vinavyotumia malighafi hususan za ndani, na kuongeza thamani, viwanda vikubwa vya mbolea na saruji, viwanda vya kanda maalum za kiuchumi, kielektroniki na TEHAMA;

iv.        Maendeleo ya rasilimali watu na Ujuzi kwa kutilia mkazo sayansi, teknolojia na ubunifu;

v.        Uendelezaji wa huduma za utalii, biashara na fedha; na

vi.        Huduma za jamii: kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii.

91.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa ugawaji wa fedha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sera ya ugatuaji wa madaraka na rasilimali. Aidha, Serikali itaimarisha mifumo ya ndani ya mapato na matumizi kwa kutoa miongozo mahsusi ya ukaguzi wa ndani, kuimarisha utendaji wa kamati za ukaguzi, kutoa mafunzo ya usimamizi na uimarishaji mifumo ya udhibiti wa ndani kwa Wakurugenzi wa Halmashauri. Vile vile, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitawezeshwa kuainisha uwezo wa pato la kila Halmashauri na fursa zilizopo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani; na kujenga uwezo wa Halmashauri katika matumizi ya mfumo wa IFMS; kuhuisha baadhi ya vyanzo vya mapato ya ndani ili kuongeza mapato; kuboresha mfumo wa uthamini wa majengo kwa kutumia kanuni za jumla; kuhamasisha Halmashauri kutumia teknolojia rahisi ya mitandao ya simu za mkononi katika kufanya malipo.

92.        Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao, Serikali itahakikisha kwamba mafungu yanapata fedha kama ilivyoidhinishwa na Bunge lako tukufu.

93.        Mheshimiwa Spika, kutokana na mashauriano ya Kamati ya Bunge ya Bajeti na Serikali, pamoja na mahitaji mengine ya Serikali jumla ya shilingi bilioni 538.6 zimeongezwa katika Bajeti hii kama mchanganuo unavyoonesha.



MCHANGANUO WA FEDHA AMBAZO ZIMETOLEWA NA SERIKALI KUPITIA
MASHAURIANO NA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 13/14

FUNGU
MAELEZO YA FUNGU
BAJETI KABLA YA NYONGEZA YA MWAKA 2013/14
FEDHA ZILIZOTOLEWA NA SERIKALI
JUMLA BAJETI YA FUNGU IKIJUMUISHA NYONGEZA
MAELEZO
15
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi
1,924,748,000
350,000,000
2,274,748,000
Fedha kwa ajili ya shughuli za usuluhishi wa migogoro ya wafanyakazi
21
Hazina
1,416,332,728,000
5,600,000,000
1,421,932,728,000
Fedha kwa ajili ya kugharamia uchambuzi wa mapato ya ziada
35
Idara ya Kurugenzi ya Mashtaka
13,011,796,000
10,000,000,000
23,011,796,000
Fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida
40
Mfuko wa Mahakama
141,696,825,000
20,000,000,000
161,696,825,000
Fedha za maendeleo
43
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
328,134,608,000
21,150,000,000
349,284,608,000

Fedha za ruzuku ya mbolea
44
Wizara ya Viwanda na Biashara
78,492,632,000
30,000,000,000
108,492,632,000
Fedha za maendeleo kwa ajili ya Kurasini Logistic Hub-EPZ Development
49
Wizara ya Maji
398,395,874,000
184,500,000,000
582,895,874,000
Fedha za matumizi ya kawaida na maendeleo kwa ajili ya miradi ya maji vijijini
53
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
21,870,448,700
2,000,000,000
23,870,448,700
Fedha za maendeleo kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake
70-95
HALMASHAURI MBALIMBALI
1,247,049,476,000
10,800,000,000
1,257,849,476,000
Matumizi ya kawaida Kutokana na ongezeko la makusanyo ya mapato kwa Halmashauri
58
Wizara ya Nishati na Madini (REA)
1,102,429,129,000
186,900,000,000
1,289,329,129,000
Fedha za maendeleo kwa ajili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
62
Wizara ya Uchukuzi
491,105,994,000
38,300,000,000.0
529,405,994,000
Fedha za maendeleo kwa ajili ya miundombinu ya Reli na Mtaji kwa TAZARA
96
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
21,328,045,000
9,000,000,000
30,328,045,000
Fedha za maendeleo kwa ajili ya kuongeza usikivu TBC shilingi bilioni 6 na Mfuko wa Maendeleo wa Vijana shilingi bilioni 3
99
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
47,180,225,000
20,000,000,000
67,180,225,000
Fedha za maendeleo kwa ajili ya maendeleo ya mifugo na uvuvi
JUMLA
5,308,952,528,700
538,600,000,000
5,847,552,528,700



94.        Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, Serikali itaongeza juhudi za kukusanya mapato ya ndani, kuharakisha majadiliano na Washirika wa Maendeleo na wakopeshaji mbalimbali katika kutafuta mikopo na misaada kwa wakati. Ninatoa wito kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba wanatimiza masharti na taratibu za kupata fedha zilizoidhinishwa na Bunge.

Mfumo Mpya wa Uandaaji na Utekelezaji wa Vipaumbele vya Miradi ya Maendeleo
95.        Mheshimiwa spika, kama ilivyoelezwa hapo awali kwenye hotuba ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais – Mahusiano na Uratibu, Mh. Stephen Masatu Wassira (Mb), Serikali imeainisha maeneo ya kimkakati ambayo yatafungua fursa ya mapinduzi ya kiuchumi na kuleta matokeo makubwa kiuchumi na kijamii kwa muda mfupi. Maeneo hayo ni utafutaji wa mapato, kilimo, maji, elimu, nishati na miundombinu ya uchukuzi. Serikali imedhamiria kutekeleza miradi kwenye maeneo hayo katika kipindi cha muda wa kati. Utekelezaji madhubuti wa vipaumbele hivi utafanikisha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati.

96.        Mheshimiwa spika, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali imeweka mikakati ya kuongeza nidhamu ya kupanga na kutekeleza miradi ya mendeleo ili kupata matokeo yanayowiana na thamani halisi ya fedha. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imeainisha maeneo makuu sita kama nilivyoeleza hapo awali ambayo yatazingatiwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Aidha, kama mnavyofahamu, Serikali imeunda chombo (Presidential Delivery Bureau) kitakachoratibu, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi katika sekta zilizobainishwa.

97.        Mheshimiwa spika, katika mwaka 2013/14, Serikali imeweka kipaumbele katika kutatua kero ya maji kwa wananchi ambapo shilingi bilioni 747.6 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini. Katika kipindi cha muda wa kati, Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama.

98.        Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi ambayo inajumuisha barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya ndege, Serikali imetenga shilingi bilioni 2,169.0 katika mwaka 2013/14 ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,940.0 mwaka 2012/13. Kati ya fedha hizo zilizotengwa mwaka 2013/14, shilingi bilioni 196.8 ni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya reli ikilinganishwa na shilingi bilioni 134.2 zilizotengwa mwaka 2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 46.6.  Aidha, Serikali imedhamiria kuongeza bajeti na kuchukua hatua za kuishirikisha sekta binafsi katika kuimarisha miuondombinu ya reli.

99.        Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza sekta ya nishati na madini, juhudi zitaelekezwa katika kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ambapo jumla ya shilingi bilioni 1,426.9 zimetengwa kwa ajili hiyo ikilinganishwa na shilingi bilioni 731.8 mwaka 2012/13.

Sekta ya Fedha
100.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itachukua hatua zifuatazo katika kuboresha sekta ya fedha:-
i.        Kutunga sheria ya Mfumo wa Malipo nchini kwa ajili ya kuwa na utaratibu wa usimamizi wa mifumo ya malipo nchini ili kuboresha matumizi ya kielektroniki katika kufanya malipo, hususan kwa kutumia simu za mikononi, huduma za benki kwa njia ya mtandao, vituo vya mauzo na mashine za kutolea fedha (ATM);

ii.        Kuandaa Sera ya Bima ya Taifa; na



iii.        Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Taasisi ndogo za Fedha, 2002.

101.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Serikali itaendelea na hatua za kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii kwa kutekeleza kazi zifuatazo:-
i.        Kuandaa kanuni na miongozo ambayo itajikita katika kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na kuifanya kuwa endelevu na yenye mchango katika maendeleo ya wanachama wa mifuko na nchi kwa ujumla;

ii.        Kusajili mifuko, mameneja uwekezaji (Fund Managers) na watunza mali (Custodians) kwa ajili ya kutenganisha majukumu kwenye uendeshaji wa Mifuko ili kuleta ufanisi zaidi; na

iii.        Kutoa elimu kwa umma kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii.

Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto
102.     Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto nilizozieleza awali, serikali imeandaa mikakati ya kukabiliana nazo katika mwaka 2013/14 kama ifuatavyo: kuhusu suala la tija katika kilimo, Serikali itaboresha mfumo wa kilimo, mifugo na uvuvi uwe wa kibiashara badala ya ule wa kujikimu; kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji; kuongeza upatikanaji na utumiaji wa pembejeo za kilimo; kuimarisha huduma za ugani; upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, kusimamia upatikanaji wa masoko; na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya kilimo.

103.     Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya fedha za umma, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wa kada za uhasibu, ununuzi, uhakiki mali na ukaguzi wa ndani. Aidha, Serikali itaimarisha, usimamizi wa mali za Serikali na kufanya uhakiki wa mali za Serikali katika Wizara, Mikoa na Halmashauri ili kuboresha daftari la mali za Serikali na kubaini mali zisizokuwa na tija kwa ajili ya kuzifuta.

104.     Mheshimiwa Spika, katika hatua za kudhibiti matumizi, Serikali itapunguza matumizi kwenye maeneo mbayo hayataathiri utoaji wa huduma za msingi. Aidha, Serikali itapitia kanuni za ununuzi ili kuhakikisha kuwa huduma na vifaa vinavyonunuliwa vinaendana na thamani ya fedha. Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika kupunguza gharama za uendeshaji.

105.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sheria ya ununuzi wa umma, kumekuwepo na kanuni za ununuzi tofauti kati ya zinazotumika katika Serikali Kuu na zile zinazotumika katika Serikali za Mitaa. Uzoefu uliopo unaonesha kuwa kanuni hizo zimekuwa na changamoto nyingi za kiutekelezaji. Ili kutatua tatizo hilo, Serikali imepanga kuoanisha kanuni za ununuzi wa umma zinazotumika katika Serikali Kuu na zile zinazotumika katika Serikali za Mitaa. Hatua hii itaboresha usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa umma. Ili kuhakikisha ununuzi wa umma unatekelezwa kulingana na Sera na Sheria husika, Wizara ya Fedha itasimamia shughuli hiyo.

106.     Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi wa Deni la Taifa, Serikali inakamilisha taratibu za kuanzisha Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa ndani ya Wizara ya Fedha ambayo itaanza kazi mwaka 2013/14. Aidha, Serikali inapitia upya Mkakati wa Kusimamia Deni laTaifa wa mwaka 2002 pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 iliyorekebishwa mwaka 2004, ili kutambua uanzishwaji wa Idara ya Kusimamia Deni la Taifa kwa mujibu wa Sheria na kuiboresha ili kwenda na wakati.

107.     Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba Bajeti ya Serikali inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, Serikali itawajengea uwezo watumiaji wa Mfumo wa Malipo (IFMS) kuhusu maeneo yaliyoboreshwa katika toleo la Epicor 9.02; kuhakikisha mihadi na malipo yote yanafanyika kwa kutumia mfumo wa IFMS; na kufanya ukaguzi wa ununuzi kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali itaweka utaratibu wa kuibua miradi, kuifanyia upembuzi yakinifu na kuichambua kabla haijatengewa fedha katika bajeti ya mwaka husika ili kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa wakati na Serikali inapata thamani halisi ya fedha.

108.     Mheshimiwa Spika, kuhusu kutumia fursa za kijiografia katika ukuzaji wa uchumi, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji hususan barabara, reli, bandari, na viwanja vya ndege; kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme; kuboresha huduma za utalii; kupunguza gharama za kufanya biashara nchini ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje; na kuimarisha ulinzi na usalama katika ngazi zote.

109.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itaendelea kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuhamasisha uzalishaji na usambazaji sawia wa mahitaji muhimu kama vile chakula, mafuta ya nishati, sukari, vifaa vya ujenzi na huduma za usafiri. Aidha, Serikali itatumia hifadhi ya taifa ya chakula kusambaza chakula katika masoko kwa ajili ya kudhibiti bei.

110.     Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, Serikali itaimarisha kamati za kisekta za kuratibu mifumo ya kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi; kuhimiza wananchi kutumia nishati mbadala; kuhamasisha wananchi kupanda mazao yanayostahimili ukame; kutumia chakula kilichopo kwa tija na uangalifu ili kukidhi mahitaji ya msingi; kuchukua tahadhari ya upatikanaji wa umeme wa uhakika; na kuelimisha wananchi wachukue tahadhari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuepuka uhaba wa chakula.


  1. MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO

111.     Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua za makusudi ili kuongeza mapato na kupanua wigo wa kodi hususan kubuni vyanzo vipya vya mapato. Aidha, itaendelea pia kupunguza misamaha ya kodi katika muda wa kati kutoka asilimia 4.3 ya Pato la Taifa katika mwaka 2011 hadi kufikia walau asilimia 1. Hivi karibuni uchambuzi wa misamaha ya kodi umeonesha kwamba, misamaha mingi ya kodi imetokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwenye maeneo ya kimkakati kupitia Kituo cha Uwekezaji. Aidha, Serikali ilisamehe kodi na ushuru kwenye mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme wa dharura na pia kusamehe kodi na ushuru kwenye uagizaji wa sukari na mchele ili kuziba pengo la upungufu wa bidhaa hizo hapa nchini. Vile vile misamaha pia imekuwa ikitolewa kwa wawekezaji katika Maeneo Maalum ambao wanazalisha bidhaa zinazouzwa nje (EPZ na SEZ), ujenzi wa miundombinu na baadhi ya miradi inayofadhiliwa na wahisani ili kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo yenye gharama kubwa kwa ukamilifu.

112.     Mheshimiwa Spika, juhudi za kupunguza misamaha zitaelekezwa zaidi katika kupunguza misamaha isiyo na tija na yenye uwezekano wa kutumika vibaya. Kwa sasa Serikali inakamilisha mapitio ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kupunguza misamaha. Aidha, Serikali inakamilisha kazi ya utafiti wa kuchambua misamaha yote ya kodi ili kuleta mapendekezo ya kupunguza misamaha isiyo na tija.

113.     Mheshimiwa Spika, kufuatia kuendelea kufanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Serikali iko katika hatua nzuri ya kukamilisha utafiti wa kuangalia vyanzo vya mapato na kuwianisha mifumo inayotumika katika ukusanyaji wa mapato hayo. Mapendekezo ya utafiti huo yatazingatiwa kwenye kipindi cha mwaka 2014/15.

114.     Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya kiuchumi na mapato katika mwaka 2013/14, ninapendekeza kufanya maboresho ya sheria mbalimbali za kodi kama ifuatavyo:

a.            Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
  1. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
  2. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
  3. Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA, 220;
  4. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
  5. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168;
  6. Sheria ya Petroli (Petroleum Act) SURA, 392;
  7. Sheria ya Uwekezaji Tanzania, SURA, 38;
  8. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;
  9. Marekebisho mengine madogo madogo katika baadhi ya sheria za kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
  10. Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.

a.            Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama ifuatavyo: -
i.        Kufuta msamaha wa VAT unaotolewa kwenye huduma za utalii chini ya Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Kipengele cha 14. Aidha, hatua hii itahusisha huduma zifuatazo: (i) Tourist Guiding (ii) Game driving (iii) Water Safaris (iv) Animal or bed watching (v) Park fees (vi) Tourist Charter Services (vii) Ground Transport. Hatua hii inalenga katika kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza misamaha ya kodi. Hata hivyo, msamaha wa ushuru wa forodha utaendelea kutolewa kwenye vifaa mbalimbali vinavyotumika katika kutoa huduma za utalii;

  1. Kutoa msamaha wa VAT kwa wazalishaji wa nguo nchini zinazozalishwa kwa pamba ya ndani kwa bidhaa na huduma zitakazotumika tu kwenye uzalishaji wa nguo hizo kupitia jedwali la tatu la Sheria ya kodi ya Ongezeko la Thamani badala ya utaratibu wa sasa wa kutoza VAT kwa wazalishaji kwa kiwango cha asilimia sifuri chini ya Jedwali la kwanza la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani “VAT”. Kwa hatua hii mzalishaji wa nguo zinazotumia pamba ya hapa nchini hatalipa VAT kwenye manunuzi ya pamba, umemr na malighafi za uzalishaji wa nguo hizo;

Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 48,977.60
  1. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332

116.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -

i.                Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 14 hadi asilimia 13. Hatua hii inalenga katika kutoa nafuu ya kodi kwa mfanyakazi;

Viwango vya sasa na vile vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -





Viwango vya sasa
Jumla ya Mapato
Kiwango cha Kodi
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 2,040,000/=
Asilimia sifuri (0%)
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 2,040,000 lakini hayazidi shilingi 4,320,000/=
14% ya kiasi kinachozidi Shilingi 2,040,000/=
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 4,320,000/= lakini hayazidi shilingi 6,480,000/=
Shilingi 319,200/= + 20% ya kiasi kinachozidi Shilingi 4,320,000/=
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 6,480,000/= lakini hayazidi shilingi 8,640,000/=
Shilingi 751,200/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi 6,480,000/=
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 8,640,000/=
Shilingi 1,291,200/= + 30% ya kiasi kinachozidi Shilingi 8,640,000/=


Viwango vinavyopendekezwa
Jumla ya Mapato
Kiwango cha Kodi
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 2,040,000/=
Asilimia sifuri (0%)
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 2,040,000 lakini hayazidi shilingi 4,320,000/=
13%  ya kiasi kinachozidi Shilingi 2,040,000/=
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 4,320,000/= lakini hayazidi shilingi 6,480,000/=
Shilingi 296,400/= + 20% ya kiasi kinachozidi Shilingi 4,320,000/=
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 6,480,000/= lakini hayazidi shilingi 8,640,000/=
Shilingi 728,400/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi 6,480,000/=
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 8,640,000/=
Shilingi 1,268,400/= + 30% ya kiasi kinachozidi Shilingi 8,640,000/=


i.                Kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni (commission) ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi. Kodi hiyo itakusanywa na kampuni za simu kutoka kwa wakala wanaotoa huduma za kusafirisha fedha kupitia simu za mkononi;

  1. Kutoza kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye malipo yatokanayo na huduma mbali mbali kama vile huduma za ushauri wa kitaalamu na nyinginezo (Consultancy services and other services). Kodi hii itatozwa bila kujali kama kuna Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi (TIN) au la. Lengo la hatua hii ni kudhibiti na kulinda mapato ya Serikali;

    1. Kutoza kodi ya zuio kwenye bidhaa zinazonunuliwa na Serikali na Taasisi zake kwa kiwango cha asilimia 2 bila kujali kama kuna Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi (TIN) au la. Lengo la hatua hii ni kudhibiti na kulinda mapato ya Serikali;

  1. Kufuta msamaha wa kodi ya zuio kwenye ukodishaji wa ndege kwa walipa kodi wasio wakazi (non-resident). Hatua hii inalenga katika kupunguza misamaha ya kodi na kuhuisha mapato ya Serikali;

Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 131,686.

  1. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147

117.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-

i.                Kuongeza kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kwenye magari yasiyo ya uzalishaji (Non-Utility Motor Vehicles) ya umri wa zaidi ya miaka 10 kutoka asilimia 20 hadi asilimia 25. Hatua hii inalenga katika kupunguza uagizaji wa magari chakavu, kulinda mazingira na kupunguza ajali;

  1. Kuanzisha kiwango kipya cha Ushuru wa Bidhaa cha asilimia 5 kwenye magari ya uzalishaji (Utility Motor Vehicles) yenye umri wa zaidi ya miaka 10 yanayotambuliwa katika HS Code 87.01, 87.02 na 87.04. Hatua hii haitahusisha magari chini ya HS Code  8701.10.00; na HS Code 8701.90.00 ambayo kimsingi ni matrekta yaliyounganishwa; na magari yasiyounganishwa chini ya HS Code 8702.10.11; 8702.10.21, 8702.10.91; 9702.90.11, 8702.90.21; 8702.90.91; HS Code 87.04; 8704.10.10; 8704.21.10; 8704.22.10; 8704.23.10; 8704.31.10, na 8704.32.10, 8704.90.10. Lengo la kuanzisha kiwango kipya cha ushuru ni kupunguza uagizaji wa magari chakavu, kulinda mazingira na kupunguza ajali. Aidha, matrekta na magari yasiyounganishwa hayatatozwa ushuru huu kwa nia ya kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya uunganishaji wa magari na hivyo kuongeza ajira na mapato ya serikali;

  1. Kurekebisha viwango vya Ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya Petroli kama ifuatavyo: -

a.            Mafuta ya Dizeli kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi shilingi 217 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 2 tu;
    1. mafuta ya Petroli kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 400 kwa lita; na,
    2. mafuta ya Taa kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 400.30 kwa lita kwa mafuta ya taa hakitabadilika;

  1. Kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia kati ya 10 hadi asilimia 25 kwenye bidhaa mbalimbali zinazozalishwa au kuingizwa nchini  kama vile; Mazulia, vipodozi, mafuta ya kujipaka, bidhaa na mifuko ya ngozi, bunduki na risasi, boti za kifahari, ndege na helikopta;

  1. Kuanzisha kiwango cha Ushuru wa bidhaa wa asilimia 15 kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, zinazotambulika katika HS Code 94.03. Hatua hii inalenga katika kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa samani kwa kutumia mbao zinazozalishwa hapa nchini. Aidha hatua hii itachochea ukuaji wa ajira na kuongeza mapato ya Serikali;

  1. Kutoza Ushuru wa bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote (all mobile phone services) za simu za kiganjani/mkononi badala ya muda wa maongezi tu (airtime alone). Katika ushuru huu asilimia 2.5 zitatumika kugharamia elimu hapa nchini.

  1. Kuongeza wigo wa kutoza Ushuru wa bidhaa kwenye huduma za simu za mezani (zinazojulikana kama simu za TTCL) na zisizokuwa na waya;

  1. Kurekebisha viwango maalum (specific rates) vya Ushuru wa bidhaa zisizokuwa za mafuta kama vile vinywaji baridi, mvinyo, pombe, vinywaji vikali, sigara n.k. kwa asilimia 10 kama ifuatavyo:-

a.            Vinywaji baridi, kutoka shilingi 83 kwa lita hadi shilingi 91 kwa lita; Hilo ni ongezeko la shilingi 8 tu kwa lita;

b.    Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (Juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini kutoka shilingi 8 kwa lita hadi shilingi 9 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 1 tu kwa lita;

c.    Ushuru wa bidhaa kwenye Juisi iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka shilingi 100 kwa lita hadi shilingi 110 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 10 kwa lita;

d.    Bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka shilingi 310 kwa lita hadi shilingi 341 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 31 kwa lita;

e.    Bia nyingine zote, kutoka shilingi 525 kwa lita hadi shilingi 578 kwa lita; yaani ongezeko la shillingi 51 kwa lita;

f.     Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, kutoka shilingi 145 kwa lita hadi shilingi 160 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 15 kwa lita moja;

g.    Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 1,614 kwa lita hadi shilingi 1,775 kwa lita. sawa na ongezeko la shilingi 161 kwa lita;

h.    Vinywaji vikali, kutoka shilingi 2,392 kwa lita hadi shilingi 2,631 kwa lita; sawa na ongezeko la shilingi 239 kwa lita moja;

i.     Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani hautaongezeka;

  1. Kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara kama ifuatavyo:-

a.            Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 8,210 hadi shilingi 9,031 kwa sigara elfu moja; sawa na ongezeko la senti 82 tu kwa sigara 1;

b.    Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 19,410 hadi shilingi 21,351 kwa sigara elfu moja; ikiiwa ni ongezeko la shilingi 1 na senti 94 kwa sigara moja;

c.    Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 35,117 hadi shilingi 38,628 kwa sigara elfu moja; ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 na senti 50 tu kwa sigara moja;

d.    Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (“cut filler’) kutoka shilingi 17,736 hadi shilingi 19,510 kwa kilo; na

e.    Ushuru wa Bidhaa kwa “Cigar” unabaki kuwa asilimia    30.

Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 510,017.50.

d. Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA, 220;

118.     Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uwezo wa Serikali katika kugharamia ukarabati wa miundo mbinu ya barabara ambayo ni muhimu katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi hapa nchini, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA, 220 kama ifuatavyo: -

i.                Kuongeza kiwango cha Ushuru wa mafuta (fuel levy) kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 263 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 63 kwa lita.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 155,893.50
  1. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
119.             Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82 kama ifuatavyo:-

  1. Kupunguza tozo ya kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi (Skills Development Levy “SDL”) kutoka kwenye kiwango cha sasa cha asilimia 6 hadi kiwango cha asilimia 5. Aidha, sambamba na kupunguza kiwango cha sasa cha SDL, Taasisi za Serikali zisizotegemea bajeti ya Serikali kwa kiwango kikubwa katika kujiendesha pia zitalipa tozo hii.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 28,213.90
  1. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168;

120.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168 ili kuongeza viwango vya Ada ya mwaka ya leseni za Magari (Annual Motor vehicle Licence Fee) kama ifuatavyo: -

i.                Gari lenye ujazo wa Injini 501.cc – 1500.cc kutoka kiwango  cha sasa cha shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000;

ii.        Gari lenye ujazo wa Injini 1501.cc – 2500.cc kutoka kiwango  cha sasa cha shilingi 150,000 hadi shilingi 200,000;

iii.        Gari lenye ujazo wa Injini zaidi ya 2501.cc kutoka kiwango  cha sasa cha shilingi 200,000 hadi shilingi 250,000.

iv.        Magari yenye ujazo wa Injini chini ya 501cc hayatatozwa  Ada ya leseni za magari.

Hatua hii itatekelezwa kupitia tangazo litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 19,710.90


g.  Sheria ya Petroli (Petroleum Act), SURA, 392;

  1. Ili kutekeleza dhamira ya Serikali ya kusambaza umeme vijijini, napendekeza kuanzisha Tozo ya mafuta ya petroli (petroleum levy) ya shilingi 50 kwa lita ambayo itakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mapato yatakayokusanywa kutoka kwenye tozo hiyo yatatumika kugharamia mahitaji ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika kusambaza umeme vijijini. Hatua hii itatekelezwa kupitia tangazo litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 123,725.

  1. Sheria ya Uwekezaji Tanzania, SURA, 38

Kutoza asilimia 25 ya ushuru wa forodha unaopaswa kutozwa kwenye bidhaa zinazotambulika kama “Deemed Capital Goods” (yaani kutoa msamaha wa kodi wa asilimia 75 kwenye bidhaa hizo badala ya asilimia 90 za sasa), na kuziondoa baadhi ya bidhaa kwenye orodha ya kupata msamaha. Bidhaa hizo ni zile ambazo hazina uasilia wa kuwa bidhaa za mtaji (capital goods) kama vile vifaa vya ofisi, samani, sukari, vinywaji (viburudisho), bidhaa za mafuta ya petroli, magari madogo (Non Utility Motor Vehicles), viyoyozi, majokofu, na vifaa vya kielektroniki, mashuka, vijiko, vikombe nk.
  1. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004

121.     Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha kutoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya Kikao cha mashauriano kuhusu masuala ya Bajeti (Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) tarehe 07 Juni 2013 mjini Arusha. Kikao hicho kilipendekeza marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC-Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.

122.     Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni:-
i.        Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano inayotambuliwa katika HS Code 1001.99.20 na HS Code 1001.99.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda na wazalishaji wa bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano hiyo;

        ii.    Kutoza ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa za mchele na sukari wakati bidhaa hizo zinapoingizwa nchini kwa msamaha maalumu wa Serikali baada ya kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Bidhaa hizo kwa sasa zinatozwa Ushuru wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa asilimia 100 kwa sukari na asilimia 75 kwa mchele.

123.     Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-

i.                Kurekebisha Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa mashine na vipuli vya reli vinavyoagizwa na Shirika la Reli Tanzania. Hatua hii inalenga katika kutoa unafuu kwenye gharama za kuboresha reli na kuimarisha usafirishaji wa reli;

ii.        Kufuta utaratibu wa kutokukagua mizigo inayoingizwa na wafanyabishara ujulikanao kama “Compliant Trader Scheme” ambao uzoefu umeonesha kwamba unatumiwa vibaya na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kulipa kodi sahihi na hivyo kuipotezea Serikali mapato yake halali;

iii.        Kuimarisha mfumo wa uthamini (valuation) wa bidhaa kutoka nje ya nchi ili kuondoa tatizo la upotevu wa mapato kutokana na uthamini usio sahihi. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa Import Export Commodity Database (IECDB);

iv.        Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa malighafi ya kutengeneza sabuni inayojulikana kama LABSA inayotambuliwa katika HS Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuimarisha uzalishaji na kukuza viwanda vidogo na vya kati vya sabuni hapa nchini;

v.        Kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye mifuko ya plastiki inayotumika katika uzalishaji wa nishati ya gesi (plastic bag biogas digesters). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kutunza mazingira;

vi.        Kuongeza ushuru wa forodha kwenye mawe yanayotumika katika mashine za kusaga bidhaa mbalimbali kutoka asilimia sifuri hadi asilimia 25. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vya Jumuiya ya Afrika Mashariki;

vii.        Kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye mitambo ya kusafisha uchafu katika maji (Water treatment effluent plant) unaotoka viwandani kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha viwanda vya ndani kutumia mitambo hii ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kupunguza gharama za uzalishaji viwandani;

viii.        Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha mwaka mmoja;

ix.        Kufanya marekebisho kwenye Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa msamaha kwa Idara ya Usalama wa Taifa.

Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 135,526.90

  1. Marekebisho mengine madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria nyingine mbalimbali.

124.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
i.        Kwa kutambua kwamba Sekta binafsi ndiyo yenye msukumo mkubwa katika maendeleo ya uchumi duniani kote, napendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya Public Procurement Act, 2011 na Public Private Partnership Act 2010 ili kuwezesha “unsolicited PPP Proposals” kutohusika na utaratibu wa ushindani ikiwa ni njia mojawapo ya kuvutia wawekezaji katika miradi ya maendeleo kwa manufaa ya kiuchumi ya nchi yetu;

ii.        Kurekebisha Sheria ya Fedha Za Umma SURA 348, Sheria ya Msajili wa Hazina SURA 418, na Sheria ya Wakala za Serikali, SURA 245, ili kuweka sharti kwa wakala na taasisi za serikali kuwasilisha kiasi cha asilimia 10 ya mapato ghafi (badala ya mapato ya ziada) ya taasisi na wakala hizo kwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

  1. Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea

125.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi.

  1. Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi

126.     Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2013, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.

  1. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2013/14
127.             Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi na shabaha ya bajeti, sura ya bajeti itakuwa kama ifuatavyo; Serikali imepanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 18,249 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje.  Mapato ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 11,154.1 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.

128.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14 Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 3,855.2. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,163.1 ni misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 2,692.1 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 500.4.

129.     Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi ya bajeti, Serikali inatarajia kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje shilingi bilioni 2,856.3. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,147.6 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na mkopo wa ndani shilingi bilioni 552.3 ambao ni asilimia moja ya Pato la Taifa na shilingi bilioni 1,156.4 ambazo ni mikopo yenye masharti ya kibiashara zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

130.     Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi, jumla ya shilingi bilioni 18,249 zimekadiriwa kutumika katika mwaka 2013/14, kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya hizo matumizi                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                            ya kawaida ni shilingi bilioni 12,574.9 ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 4,763 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Taasisi na Wakala za Serikali; Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi bilioni 3,319.2, na Matumizi Mengineyo shilingi bilioni 4,492.6.

131.     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013/14 jumla ya shilingi bilioni 5,674 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2,982 kitagharamiwa kwa fedha za ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 552.3 zinatokana na mkopo kutoka vyanzo vya ndani, shilingi bilioni 1,156.4 ni mikopo ya masharti ya kibiashara, shilingi bilioni 386.2 ni mikopo ya kibajeti, na shilingi bilioni 887.1 zitatokana na asilimia 8 ya mapato ya kawaida. Kiasi cha shilingi bilioni 2,692.6 kitagharamiwa kwa fedha za nje, misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha Mifuko ya Pamoja ya Kisekta.


132.     Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, mfumo wa bajeti kwa mwaka 2013/14 unakuwa kama ifuatavyo:

Mapato
Shilingi Milioni

A.
Mapato ya Ndani

11,154,071

(i)   Mapato ya Kodi (TRA)
10,412,937


(ii)  Mapato yasiyo ya Kodi
741,134





B.
Mapato ya Halmashauri

383,452
C.
Mikopo na Misaada ya Kibajeti

1,163,131
D.
Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo ikijumuisha MCA (T)

2,692,069
E.
Mikopo ya Ndani

1,699,860
F.
Mikopo yenye Masharti ya Kibiashara

1,156,400





JUMLA YA MAPATO YOTE

18,248,983





Matumizi


G.
Matumizi ya Kawaida

2,574,949

(i)    Deni la Taifa
3,319,156


(ii)   Mishahara
4,763,196


(iii)  Matumizi Mengineyo
4,492,566


Wizara                       3,738,316



Mikoa                             49,701



Halmashauri                     04,549


H.
Matumizi ya Maendeleo

5,674,034

(i)  Fedha za Ndani
2,981,965


(ii)  Fedha za Nje
2,692,069


JUMLA YA MATUMIZI YOTE

18,248,983


  1. HITIMISHO
133.             Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, bajeti ya mwaka 2013/14 imelenga kutekeleza Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa miaka mitano; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na kuanza kutekeleza maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Labs. Madhumuni ya mipango na mikakati hii ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

134.     Mheshimiwa Spika, suala ambalo ningependa kulisisitiza ni sote kwa pamoja kuongeza ushirikiano katika kusimamia majukumu na matumizi ya fedha na rasilimali zetu vizuri ili kuongeza ufanisi. Masuala yote tuliyoyajadili katika bunge hili ni ya msingi sana, hivyo kama yakifanyiwa kazi kwa ufanisi tutafikia matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo yanalenga kuitoa Tanzania katika kundi la nchi maskini na kuingia katika kundi la nchi zenye viwango vya kati vya mapato na hali bora ya maisha.

135.     Mhesimiwa Spika, bajeti hii imelenga pia kuongeza makusanyo ya mapato, hasa ya ndani kwa kuanzisha vyanzo vipya na kuboresha vilivyopo. Lengo likiwa ni kujitosheleza kwa mapato yatakayowezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi. Katika kikao hiki cha Bunge la bajeti, waheshimiwa wabunge walipendekeza kuongeza fedha kwa baadhi ya mafungu ili kuyawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali sikivu ya Chama cha Mapinduzi imezingatia kwa kiasi kikubwa mapendekezo hayo. Ili kutekeleza mapendekezo hayo, imelazimu kufanya maboresho zaidi katika kodi na tozo mbalimbali kwani isingewezekana kugharamia mapendekezo hayo bila kuathiri upande wa kodi. Hivyo, waheshimiwa wabunge naomba mnielewe katika hili na kuniunga mkono ili mafungu yaweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kufikia malengo tuliojiwekea.

136.     Mhesimiwa Spika, Serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha miundombinu ya kiuchumi, kifedha na kijamii ili kuongeza fursa za ushiriki wa wananchi katika uzalishaji na kuboresha hali zao za maisha. Bajeti, inalenga pia kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika, kuendeleza ardhi na kuunganisha nchi yetu kwa njia ya miuondombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege na mawasiliano. Hii itasaidia pia kutumia vyema fursa za kijiografia zinazotokana na kupakana na nchi zisizokuwa na bahari. Aidha, bajeti hii inalenga kufungua fursa za kuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu kupitia mfumo mpya wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ambapo italeta matokeo makubwa kwa haraka.

137.     Mheshimiwa Spika, bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14 imezingatia mapendekezo ya Kamati ya Bajeti na Kamati za Kisekta za Bunge kadiri hali ya fedha ilivyoruhusu. Ushauri uliotolewa na Kamati hizo na hoja mbalimbali zilizotolewa na waheshimiwa wabunge zilifanyiwa kazi kadiri ilivyowezekana. Aidha, kwa utaratibu huu mpya wa mzunguko wa bajeti ambao ulipitisha bajeti za mafungu mbalimbali, maelelezo yangu haya ni kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14.
138.               Mheshimiwa Spika, yote niliyoyasema yanawezekana iwapo kila mmoja wetu na wananchi kwa ujumla tutatimiza wajibu wetu, kila mmoja kwa nafasi yake, kwa kushiriki na kuwajibika kikamilifu katika kutekeleza sera na mipango tuliyojiwekea.


Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja

No comments:

Post a Comment